Maafisa Utawala na Rasirimali Watu 316 nchini wapimwa moyo
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Saturday, May 09, 2026
Jumla ya maafisa Utawala na Rasirimali Watu 316 nchini wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kuwawezesha kufahamu namba zao na kuwapa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo.
Uchunguzi huo umefanyika kwa siku tatu wakati wa Mkutano Mkuu wa pili Jumuishi wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma Tanzania uliomalizika jana katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Akielezea kuhusu mwitikio wa maafisa hao kufanya uchunguzi wa afya Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Salehe Mwinchete alisema mwitikio umekuwa mkubwa na wenye tija kwa maafisa Utawala na Rasirimali Watu nchini.
“Baada ya kuwafanyia uchunguzi wa afya baadhi ya maafisa Utawala na Rasirimali Watu tumewapa rufaa kufika katika Hospitali zetu kwaajili ya uchunguzi zaidi kutokana na kuona viashiria ambavyo vinahitaji uchunguzi zaidi”, alisema Dkt. Salehe
Dkt. Salehe alisema inapotokea fursa kama hiyo ya kupima afya eneo la kazi ni vizuri watumishi wakaitumia vizuri kwani wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi wanakosa muda wa kufika hospitali kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya.
“JKCI tumekuwa mstari wa mbele kuwafikishia watumishi wa umma na sekta binafsi huduma za uchunguzi wa afya wakati wa mikutano mbalimbali lakini pia hata kuwafuata katika maeneo yao ya kazi, jitihada zote hizi tunazofanya tunataka kuhakikisha kuwa tunailinda jamii na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo”, alisema Dkt. Salehe
Nao maafisa Utawala na Rasirimali Watu walioshiriki katika mkutano huo wameiomba JKCI kuendela kutoa elimu ya magonjwa ya moyo ili kuliokoa taifa la Tanzania na changamoto ya magonjwa hayo.
Maafisa hao walisema Serikali ya Tanzania ina mchango mkubwa katika kuhakikisha watu wake wanakuwa salama ndio maana imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya na kuhakikisha elimu kuhusu kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali inawafikia wananchi.