Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Mkazi wa Temeke apongeza huduma za upasuaji wa moyo alizofanyiwa JKCI

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, Jun 18, 2026
image description

Mkazi wa Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam Jonathan Mwanayongo ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kufanikisha upasuaji mkubwa wa moyo uliokuwa ufanyike nchini India.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hii Jonathan alisema  amegundulika kuwa na matatizo la moyo mwaka huu na baada ya kufanyiwa uchunguzi wa afya alibainika kuwa alikuwa na tatizo la kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo iliyohitaji upasuaji wa haraka ili kuokoa maisha yake.

Jonathan alisema baada ya kufikishwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipokelewa na timu ya wataalamu mabingwa bobezi ambao walimfanyia uchunguzi wa kina na kuanza maandalizi ya matibabu kabla ya kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo ulioshirikisha madaktari bingwa kutoka JKCI na Hospitali ya Jaslok ya nchini India.

“Ulikuwa ni upasuaji mkubwa ambao kwa kweli hatukuamini kama ungeweza kufanyika hapa Tanzania hivyo nilikuwa nimeanza kufanya mpango wa kwenda nje ya nchi lakini baada ya kukutana na wataalamu wa JKCI walinishauri kuwa matibabu hayo yanafanyika hapa  nchini na kweli nimefanyiwa upasuaji na sasa naendelea vizuri”, alisema Jonathan.

Jonathan aliongeza kuwa kwa sasa anaendelea vizuri kiafya baada ya kufanyiwa upasuaji huo na kwamba ameridhishwa na huduma alizopata katika Taasisi hiyo ikiwemo huduma za wauguzi, madaktari na wataalamu wengine wote waliomhudumia.

“Nawaomba watanzania wenzangu tusiwe na sababu za kwenda nje ya nchi kwaajili ya matibabu ya moyo kwani huduma hizi zipo hapa nchini na JKCI inafanya vizuri katika kuhakikisha inaokoa maisha ya watanzania”, alisema Jonathan.


Jonathan amewashukuru madaktari, wauguzi na watumishi wa JKCI kwa huduma bora na kujitolea kwao akisisitiza kuwa taasisi hiyo ina uwezo mkubwa wa kutoa huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi katika matibabu ya moyo nchini.