JKCI yasaini makubaliano na China ujenzi wa hospitali mpya ya moyo
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Wednesday, Jun 17, 2026
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Wataalamu kutoka China wasaini hati ya makubaliano ujenzi wa hospitali mpya ya moyo itakayoleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa wagonjwa wa moyo nchini.
Hati hiyo imesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge pamoja na Kiongozi wa Kamati ya Ukaguzi wa Mradi kutoka Jamhuri ya Watu wa China Yang Ling na kuahidi kuanza mchakato wa ujenzi huo mara baada ya taratibu kukamilika.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji wa saini Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema hospitali hiyo itasaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa, pamoja na kuimarisha mazingira ya kazi kwa wataalamu wa afya wanaofanya kazi katika Taasisi hiyo.
“Mradi huu ni hatua muhimu sana katika kuimarisha uwezo wetu wa kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa viwango vya juu zaidi na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma bora kwa wakati”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema mradi huo ni sehemu ya juhudi ya Serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya afya na kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.