Prof. Kabudi; Watanzania jivunieni kuwa na JKCI, Ni Taasisi ya umahiri Barani Afrika
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Saturday, Jul 04, 2026
Watanzania wametakiwa kujivunia uwepo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwani ni taasisi ya umahiri katika Bara la Afrika inayotoa huduma za kisasa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa viwango vya kimataifa.
Wito huo umetolewa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Prof. Palamagamba Kabudi alipotembelea banda la JKCI katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (SABASABA) ambapo aliwataka watanzania kuitumia taasisi hiyo na kuiunga mkono hususan katika kampeni yake ya kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo ili waweze kupata matibabu na kuendelea kutimiza ndoto zao.
Prof. Kabudi aliipongeza JKCI kwa huduma zake za kisasa za tiba ya moyo, akisema ameridhishwa na kiwango cha utaalamu alichokiona pamoja na uwepo wa wataalamu wabobezi wanaotoa huduma na elimu kwa wananchi katika maonesho hayo hatua ambayo inaonesha dhamira ya taasisi hiyo ya kuwafikia watanzania popote walipo na kuwapatia huduma za kibingwa.
Aidha Prof. Kabudi alizitaka hospitali nyingine nchini kuiga kampeni ya “Jua Namba Zako” ambayo inalenga kuwahamasisha wananchi kufahamu viashiria muhimu vya afya zao ili kusaidia kinga na utambuzi wa mapema wa magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza.
Prof. Kabudi alisisitiza kuwa huduma zinazotolewa na JKCI ni za kiwango cha juu na zinawafikia watanzania wa makundi yote bila ubaguzi hivyo kuimarisha afya ya jamii na kuongeza uelewa kuhusu kinga na matibabu ya magonjwa ya moyo.