JKCI yapongezwa kwa kutoa huduma bora kwa wateja katika maonesho ya SABASABA
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Saturday, Jul 04, 2026
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ubunifu na kuwa darasa muhimu la elimu ya afya na mfano wa utoaji wa huduma bora kwa wateja katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (SABASABA).
Dkt. Ulisubisya alisema kutembelea kwake katika banda la JKCI kumemfungua macho kuona namna huduma zinazopatikana hospitalini zinavyoweza kutolewa katika maonesho bila kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi wanaohitaji matibabu katika taasisi hiyo kwani JKCI imejipanga vizuri kupokea wananchi na kutoa huduma mbalimbali ikiwemo vipimo kwa ubora unaolingana na huduma zinazotolewa katika matawi yake.
Aidha Dkt. Ulisubisya alisema uchangamfu na weledi wa wataalamu wa JKCI umemvutia akieleza kuwa kwa sasa taasisi nyingi zinahitaji kuimarisha huduma bora kwa wateja kama ambavyo JKCI inafanya kwani kila anayefika katika banda hilo hupokelewa vizuri, kupewa maelezo ya kutosha na kuondoka akiwa amepata elimu ya kina kuhusu magonjwa ya moyo pamoja na umuhimu wa lishe bora.
“Uwepo wa banda la JKCI katika maonesho haya ni hatua muhimu ya kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kuchunguza afya zao mara kwa mara badala ya kusubiri hadi wanapougua ndipo waende hospitalini kwani elimu inayotolewa katika banda hili inaweza kusaidia kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu kinga na utambuzi wa mapema wa magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Ulisubisya.