Wizara ya Afya, JKCI na Children’s HeartLink waweka mikakati ya kuimarisha huduma za moyo kwa watoto nchini
-
Author:
JKCI Admin
-
Published At:
Saturday, Jun 27, 2026
Serikali kupitia Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Shirika la Children’s HeartLink na Shirika la Afya Duniani (WHO) waweka mikakati ya kitaifa kuimarisha huduma za matibabu ya moyo kwa watoto kuhakikisha kila mtoto mwenye ugonjwa huo anagundulika mapema, anapata matibabu kwa wakati na kuongeza nafasi ya kuishi.
Akizungumza wakati wa mkutano uliofanywa na wadau hao jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema ushirikiano huo umewakutanisha wataalamu na wadau hao ili kujadili njia bora za kuboresha huduma za moyo kwa watoto nchini na katika ukanda wa Afrika.
Dkt. Kisenge alisema mkutano huo umelenga kutengeneza mikakati ya kushirikiana na Serikali ili kuondoa vikwazo vinavyowafanya watoto kushindwa kupata matibabu kutokana na gharama, ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa rasilimali fedha na kuendeleza ajenda ya bima ya afya kwa wote.
“Wadau hawa pia wamekusudia kubadilishana uzoefu na ujuzi kwa kutumia mafanikio yaliyopatikana JKCI kama mfano wa kuigwa katika nchi nyingine huku wakijenga uwezo wa wataalamu kupitia mafunzo ya kugundua mapema magonjwa ya moyo kwa watoto na kuimarisha tafiti zitakazosaidia kubaini sababu za magonjwa hayo pamoja na njia za kuyazuia”, alisema Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani alisema mkutano huo umekuwa jukwaa muhimu lililowakutanisha wadau wa sekta ya afya nchini pamoja na washirika wa maendeleo kutoka Marekani kwa lengo la kuandaa mpango madhubuti wa kitaifa wa kuhudumia watoto wenye magonjwa ya moyo.
Dkt. Naizihijwa alisema kupitia uzoefu wa washirika hao Tanzania itaweza kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma ili kuhakikisha watoto wanaohitaji matibabu wanayapata kwa haraka, kwa ubora na kwa uhakika bila kujali mahali walipo.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya Dkt. Omary Ubuguyu alisema mkutano huo umejikita katika kujadili magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo pamoja na yale yanayotokea baada ya kuzaliwa ambayo mara nyingi hayapewi kipaumbele vya kutosha.
Dkt. Ubuguyu alisema baada ya mkutano huo wadau hao wametoka na maazimio matatu muhimu ikiwemo kuweka mikakati ya pamoja ya kupata rasilimali fedha, wataalamu na vifaa vya tiba kuanzia ngazi ya jamii hadi hospitali za rufaa, kuboresha mifumo ya kugundua wagonjwa ya moyo katika hatua za awali ili watoto waweze kupata huduma mapema, na kuunda timu ya uratibu itakayosimamia utekelezaji wa maazimio yote yaliyofikiwa.
Akihitimisha Makamu wa Rais Mkakati wa Kimataifa na Utetezi Shirika la Children’s HeartLink Bistra Zheleva alisema shirika hilo limekuja Tanzania kushirikiana na Wizara ya Afya na JKCI katika kupanua huduma za magonjwa ya moyo kwa watoto na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo.
Bistra alisema lengo kuu la ushirikiano huo ni kuhakikisha huduma za moyo zinawafikia watoto wote nchini kwa wakati ili kila mtoto mwenye ugonjwa wa moyo apate matibabu stahiki, aishi maisha yenye afya na aweze kufikia uwezo wake kamili.
“Kupitia ushirikiano huu tuliouanzisha na Tanzania tumepata nafasi kubwa ya kujenga mfumo imara na endelevu wa huduma za moyo kwa watoto ambao unaweza kuwa mfano kwa nchi nyingine Barani Afrika”, alisema Bistra