Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Wataalamu kutoka nchini Namibia watembelea JKCI kuona huduma zinazotolewa

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, Jun 25, 2026
image description

Ujumbe wa viongozi, wataalamu wa afya na wafanyabiashara kutoka nchini Namibia watembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuangalia huduma zinazotolewa pamoja na kujifunza ili iweze kuanzisha ushirikiano wa kuwaleta wagonjwa wa nchini humo kupata huduma katika Taasisi hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji wa JKCI Dkt. Angela Muhozya alisema wataalamu hao wameweza kujifunza na kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika Taasisi hiyo. 

“Nchini Namibia hakuna Taasisi kama yetu inayotoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo hivyo wakaona ni muhimu wakaja kujifunza kwetu na kuangalia namna ya kushirikiana katika kutoa huduma bingwa bobezi za moyo kwa wananchi wa Namibia”, alisema Dkt. Angela.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Uwekezaji na Maendeleo kutoka nchini Namibia (NIPDB) Jessica Hauuanga alisema maendeleo yaliyopo katika Sekta ya Afya nchini Tanzania yamewavutia kwani Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta hiyo.

Jessica alisema Serikali ya Tanzania imeweza kuwasaidia wananchi wake kupata huduma za kibingwa bobezi karibu na nyumbani hatua ambayo imeweza kuwarahisishia wananchi wake na kupunguza gharama za matibabu kwa kuzifuata nje ya nchi.

"Leo tumeweza kujionea kwa macho namna ambavyo Tanzania inafanya katika sekta ya afya, tulichokiona hapa leo kinaonyesha kuwa maendeleo yanawezekana si kwa nadharia pekee bali kwa vitendo”, alisema Jessica

Jessica aliongeza kuwa uzoefu walioupata katika Taasisi hiyo utawasilishwa kwa viongozi wa sekta ya afya wa nchini Namibia ili kusaidia mipango ya kuboresha huduma za afya na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.