JKCI kuanzisha kampuni tanzu kuimarisha tiba utalii nchini
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Thursday, Jun 25, 2026
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepanga kuanzisha kampuni tanzu itakayojikita katika shughuli za tiba utalii, kuwezesha upatikanaji wa vifaa tiba na huduma nyingine za kimkakati kwa lengo la kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti Msaidizi wa Kamati ya Maandalizi ya Mpango Mkakati wa tatu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wa mwaka 2026/27 mpaka 2030/2031 Iddi Lemah wakati wa kuwasilisha mpango mkakati huo kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo jana jijini Dar es Salaam.
Lemah alisema mpango mkakati huo umeandaliwa na kuwashirikisha kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo ili kuhakikisha kila mmoja anaelewa malengo ya Taasisi na kushiriki katika utekelezaji wake.
“Mpango mkakati huu utawanufaisha wafanyakazi kwa sababu ndio njia ya kujipima yale malengo ambayo tumejiwekea tunayafikia katika kipindi cha miaka mitano na namna gani tutashirikiana kuendeleza huduma hizi bingwa bobezi za moyo”, alisema Lemah.
Lemah alisema moja ya maeneo mapya yaliyowekwa katika mpango mkakati huo ni pamoja na kuanzishwa kwa kampuni tanzu itakayosaidia kuongeza ufanisi wa taasisi katika maeneo mbalimbali ya kimkakati.
“Kampuni tanzu hiyo itashughulika na tiba utalii, ununuzi wa vifaa tiba pamoja na kushirikiana na kampuni mbalimbali za nje ya nchi katika upatikanaji wa vifaa tiba”, alisema Lemah.
Kwa upande wake Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Tunzo Lundgreen alisema mpango mkakati huo umewekwa malengo ambayo yanayotekelezeka hivyo ni muhimu wafanyakazi wakashirikiana kwa pamoja kufanya kazi kwa ufanisi.
“Mpango mkakati wa mwaka 2026/27 mpaka 2030/2031 umehusisha mambo yote muhimu ambayo Taasisi inafanya kwa kuzingatia masuala uendelevu ya upanuzi wa Taasisi, utalii tiba, masuala ya fedha pamoja na utawala bora”,
“Kama Taasisi itasimamia vizuri rasilimali zake na kuendeleza ubunifu mbalimbali uliowekwa kwenye mpango mkakati huu itaongeza kipato na kuimarisha huduma zake katika kipindi cha miaka mitano ijayo”, alisema Tunzo.
Mpango mkakati huo unatarajiwa kuwa dira ya maendeleo ya JKCI katika kipindi cha miaka mitano ijayo kwa kuimarisha huduma za matibabu ya moyo, kuendeleza tiba utalii na kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali zilizopo.