Shilingi bilioni 500 zaokolewa matibabu ya moyo kufanyika nchini.
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Monday, May 25, 2026
Serikali kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 500 fedha ambazo zingetumiwa na Serikali kupeleka wagonjwa wa moyo kutibiwa nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa hafla fupi iliyofanyika leo katika ukumbi wa Taasisi hiyo kuzindua kampeni ya kitaifa ya kuchangisha fedha kwaajili ya matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo ijulikanayo “Kutoa ni Moyo” inayofanywa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF).
Dkt. Kisenge alisema JKCI imeshawafanyia upasuaji wa moyo watoto 3,500 lakini bado uhitaji ni mkubwa kwani wapo watoto zaidi ya 1,500 wanasubiria kufanyiwa upasuaji wa moyo ambao unagharimu kiasi cha shilingi milioni nane hadi 15 kwa mtoto mmoja.
“Tangu Taasisi hii imeanzishwa kumekuwa na mabadiliko makubwa katika masuala ya tiba ya moyo na upasuaji wa moyo, JKCI sasa hivi inafanya upasuaji wa moyo wa aina mbalimbali, kupitia uwekezaji uliofanywa na Serikali sasa hivi alisilia 97 ya magonjwa ya moyo kwa watoto yanafanyiwa upasuaji katika Taasisi yetu”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema nia ya JKCI ni kuhakikisha kuwa hamna mtoto yoyote ambaye anatoka katika familia masikini anapata changamoto ya matibabu ya moyo, kwani JKCI kwa kushirikiana na HTAF wameweka mikakati ya kuhakikisha watoto hao wanapata matibabu na dawa kuhakikisha kuwa wanajenga taifa la kesho lililo na afya njema.
“Namshukuru sana Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyotoa fedha nyingi kugharamaia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo, amekuwa akigharamia zaidi ya alisimia 70 ya matibabu ya watoto hao”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema kupitia kapeni ya kitaifa ya Kutoa ni Moyo inayofanywa na HTAF, JKCI inatamani kuona kila mtanzania mwenye uwezo anachangia matibabu ya watoto wanaotoka katika familia duni na kuwapa furaha watoto hao kwani kutoa ni moyo na wakitoa kwa moyo mmoja watajenga taifa lijalo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Heart Team Africa Foundation (HTAF) Dkt. Naizihijwa Majani alisema watoto 405 wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI wameweza kupatiwa matibabu kupitia mfuko wa HTAF.
Dkt. Naizihijwa alisema kupitia gala dinner iliyofanywa na Taasisi hiyo shilingi bilioni 2.7 zilikusanywa kutoka kwa wadau na baadaye kuendelea kukusanya ambapo hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 3.3 zimekusanywa na Taasisi hiyo kugharamia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo.
“Tunatoa shukrani za dhati kwa wadau wote waliotuunga mkoni katika gala dinner iliyofanyika mwaka 2024, tulipata mshikamano mkubwa kutoka kwa watanzania, taasisi, makampuni, wafanyabiashara, na marafiki wa watoto wenye magonjwa ya moyo ambao kila mmoja aliweka mkono wake kufanikisha matibabu ya watoto hao”, alisema Dkt. Naizihijwa
Dkt Naizihijwa alisema nyuma ya kila mchango kuna maisha ya mtoto, kuna furaha ya familia na tumaini jipya la kesho, watoto wengi wenye magonjwa ya moyo kama hawatafanyiwa upasuaji mapema wanaweza wasisherehekee siku yao ya kuzaliwa ya mwaka mmoja na wengine wengi watashindwa kusherehekea siku yao ya kuzaliwa wakiwa na miaka mitano lakini wanapohudumiwa mapema maisha yao hubadilika kabisa na kupona.
Dkt. Naizihijwa aliongeza kuwa mahitaji bado ni makubwa, kila mwaka wanazaliwa watoto takribani elfu 16 wenye matatizo ya moyo hapa nchini ambapo karibu watoto 4,000 huitaji matibabu na upasuaji wa haraka ili kuokoa maisha yao.
“Kupitia HTAF tunaendelea kushirikiana na JKCI kuhakikisha watoto wengi zaidi wanapata nafasi ya kuishi, kusoma, kucheza, na kutimiza ndoto zao, ndio maana leo tunazindua rasmi kampeni yetu ya kitaifa ya Kutoa ni Moyo kuhamasisha watanzania wote wanashiriki kusaidia watoto hawa kupata matibabu yao kwa wakati”, alisema Dkt. Naizihijwa