Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Ushirikiano na Jamii waongeza nguvu ya matibabu ya Moyo JKCI

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Saturday, Mar 14, 2026
image description

Jamii na wadau mbalimbali wametakiwa kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuleta marafiki na washirika watakaosaidia taasisi hiyo kufikia malengo yake ya kutoa huduma bingwa na bobezi za matibabu ya moyo kwa watoto.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ushirikiano kati ya JKCI na taasisi isiyo ya kiserikali ya Moyo Mission uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Dkt. Naizihijwa ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto alisema ushirikiano huo unaoenda sambamba na ujio wa wataalamu wa afya ya moyo kutoka Ujerumani unalenga kuongeza uwezo wa taasisi hiyo katika kutoa huduma za kibingwa na kibobezi za moyo hususan katika upasuaji wa moyo kwa watoto.

"Lengo kubwa la ushirikiano huu ni kubadilishana uzoefu na kusaidia kufanya upasuaji kwa watoto wengi kwa muda mfupi. Tunatarajia kuwafanyia upasuaji wa moyo watoto kati ya 10 hadi 15 ndani ya siku tano", alisema Dkt. Naizihijwa.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo na Mishipa ya Damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Joseph aliipongeza taasisi ya Moyo Mission kwa kuchagua kushirikiana na JKCI katika juhudi za kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo.

"Kupitia ushirikiano huu na madaktari kutoka Ujerumani, tutahakikisha tunatoa huduma za kibingwa na kibobezi kwa kutumia rasilimali zilizopo ili watoto wapate matibabu bora", alisema Dkt. Joseph.

Naye Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo kutoka Ujerumani, Daniel Briemann aliishukuru JKCI kwa kukubali kushirikiana nao katika kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto.

"Tunafurahi kuwa sehemu ya juhudi za kuwahudumia watoto wa Tanzania wenye matatizo mbalimbali ya moyo. Lengo letu ni kuwafikia wagonjwa wengi zaidi na kuokoa maisha yao", alisema Dkt. Briemann.

Kwa upande wake msanii wa muziki wa kizazi kipya Bernard Paul maarufu kama Ben Pol ambaye pia ni rafiki wa karibu wa JKCI na Moyo Mission aliwataka wadau mbalimbali kujitokeza kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za matibabu ya moyo kwa watoto.

"Kazi kubwa inayofanywa na Moyo Mission ni kutafuta wadau watakaoshirikiana na JKCI katika kutoa matibabu ya moyo na kuokoa maisha ya watoto wengi", alisema Ben Pol.