Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Kamati ya Bunge yasifu uwekezaji wa Serikali katika JKCI

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Saturday, Mar 14, 2026
image description

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imetambua uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya ikiwemo Taasisi ya Moyo ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kusema kuwa umeleta matokeo chanya katika kuboresha matibabu ya kibingwa ya moyo nchini.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt. Johannes Lembulung Lukumay wakati akitoa majumuisho ya ziara ya kamati hiyo walipotembelea  JKCI kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na uwekezaji uliofanywa na serikali katika taasisi hiyo.
Kamati hiyo pia  imeipongeza JKCI kwa juhudi zake za kuboresha huduma za moyo kwa watu wazima na watoto pamoja na kufungua matawi ya matibabu ya moyo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwafikia wananchi karibu zaidi.
“Uwekezaji uliofanywa hapa JKCI na Mhe. Rais Dkt. Samia ni mkubwa na wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 13, ukijumuisha jengo jipya la watoto na vifaa tiba vya kisasa ikiwemo maabara na mitambo kama Cathlab. Huu ni uwekezaji unaoonyesha dhahiri  na umuhimu wa Serikali katika kuimarisha sekta ya afya”, alisema Mhe. Dkt. Lukumay.
Mwenyekiti huyo wa kamati aliongeza kuwa JKCI ni miongoni mwa taasisi zinazofanya vizuri nchini na barani Afrika katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo akitaja pia juhudi za uongozi wa taasisi hiyo katika kupanua huduma zake ikiwemo kufungua vituo vya matibabu ya moyo katika hospitali mbalimbali nchini kama vile Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC).
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi alisema uwekezaji uliopo JKCI unasaidia kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo na umeonesha  dhamira ya Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata matibabu ya moyo ya kisasa na bora.
Aliongeza kuwa mwaka jana jumla ya watoto 350 wamefanyiwa upasuaji wa moyo bila gharama yoyote  upasuaji ambao umegharamiwa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali huduma hizo zimeokoa maisha ya watoto wengi na kuonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau katika kuboresha huduma za afya.
Mhe. Dkt. Samizi aliwapongeza watendaji wa JKCI kwa juhudi zao za kuboresha huduma za moyo kwa watoto na watu wazima huku akiwahimiza watanzania hasa wale wenye changamoto za kiafya kwa watoto kuwapeleka  mapema katika taasisi hiyo ili waweze kupata matibabu mapema ikiwa ni njia ya kuhakikisha maisha yao yanaokolewa.
“Ninawapongeza JKCI kwa kutumia teknolojia za kisasa katika tiba, ikiwemo maabara na mitambo ya upasuaji, iliyoongeza muda wa kutoa matokeo na kuhakikisha matokeo hayo ni ya uhakika. Tunaona wazi kuwa JKCI imekuwa kitovu cha matibabu ya moyo nchini kwa kutoa huduma kwa wananchi bila kulazimika kwenda kutibiwa nje ya nchi”,  alisema Dkt. Samizi.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI,  Dkt. Peter Kisenge alisema taasisi hiyo imeendelea kupanua huduma zake za matibabu ya moyo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi ndani na nje ya Tanzania.
Dkt. Kisenge alisema JKCI kwa sasa inatoa huduma mbalimbali za kibingwa na bobezi za matibabu ya moyo ikiwemo upasuaji wa moyo kwa watoto na watu wazima, upasuaji wa moyo kwa kutumia tundu dogo, matibabu ya mishipa ya damu ya moyo, matibabu ya umeme wa moyo, kupandikiza vifaa visaidizi vya moyo pamoja na huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa kutumia vifaa vya kisasa vya picha za moyo.
“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu ya moyo hapa hapa nchini bila kulazimika kwenda nje ya nchi. Tumekuwa tukipanua huduma zetu kwa kufungua matawi katika maeneo mbalimbali pamoja na kuimarisha miundombinu na teknolojia ya kisasa ili kuongeza ubora wa huduma”,  alisema Dkt. Kisenge.
Aliongeza kuwa taasisi hiyo pia inaendelea kuwekeza katika mafunzo ya wataalamu wa ndani ili kuongeza idadi ya madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa ya moyo nchini hatua ambayo itasaidia kuongeza uwezo wa kutoa huduma hizo kwa wananchi wengi zaidi.
Kamati hiyo ya Bunge imeiagiza wizara husika kuipatia JKCI eneo zaidi litakalowezesha taasisi hiyo kupanua miundombinu na kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za matibabu ya moyo ili wananchi wengi zaidi wapate huduma za  matibabu ya moyo ya kisasa na bora bila kulazimika kwenda nje ya nchi.