• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

JKCI kushirikiana na Shirika la Humaniti la Canada kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto Zanzibar

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Friday, Aug 15, 2025
image description

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) itashirikiana na Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na huduma za kibinadamu la Humaniti lililopo nchini Canada katika kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto  waliopo Visiwani Zanzibar.

Ushirikiano huo utawasaidia watoto wenye matatizo ya moyo waliopo visiwani humo kupata huduma za matibabu kwa wakati na hivyo kuokoa maisha yao.

 Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akiongea na viongozi wa Shiriki hilo walipotembelea taasisi hiyo kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.

“Ninaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Taasisi yetu, kupitia uwekezaji huu hawa wenzetu kutoka nchini Canada wameona waje kushirikiana na sisi katika kutoa huduma ya matibabu ya moyo kwa watoto waliopo Zanzibar”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema wataalamu wa JKCI  wamekuwa wakienda Visiwani Zanzibar kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto, kuwepo kwa ushirikiano huo kutawezesha kupatikana kwa huduma hizo mara kwa mara.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Humaniti Firaaz Azeez alisema mwaka 2024 akiwa na wataalamu kutoka Shirika la Muntada Aid la nchini Uingereza kupitia mradi wa Little Heart walifika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto na kujionea vifaa tiba vya kisasa na wataalamu wabobezi  waliopo JKCI.

 “JKCI ni kituo cha umahiri cha matibabu ya moyo katika nchi za Afrika ya Mashariki na Kati tumeona tushirikiane nao katika kutoa huduma za matibabu kibingwa ya  moyo kwa watoto waliopo Zanzibar na nchi zingine za Afrika”.

“Tutashirikiana nao kwa kufanya  upimaji, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya waliopo Zanzibar na kutoa uelewa kwa umma kuhusu magonjwa ya moyo kwa watoto ili watoto wenye matatizo haya waweze kutambuliwa mapema na kupata huduma kwa wakati”, alisema Azeez.