Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

JKCI Yatoa Rai kwa Watumishi Kuongeza Ufanisi na Weledi Kazini

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Friday, Mar 20, 2026
image description

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na moyo wa kujituma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na kuchangia kuboresha sekta ya afya nchini.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati wa kikao cha wafanyakazi kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa JKCI jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kisenge alisema licha ya mafanikio yaliyofikiwa na taasisi hiyo  katika utoaji wa huduma bado kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza juhudi na kujitoa zaidi kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za matibabu mbalimbali.

“Kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa ndani na nje ya nchi ambapo wagonjwa kutoka nje wamefikia 87 kwa mwezi. Hali hii inahitaji huduma kutolewa kwa viwango vya kimataifa pamoja na kupunguza msongamano. Ninawaomba wafanyakazi mniunge mkono katika juhudi hizi za kuhakikisha JKCI inaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi”,  alisema Dkt. Kisenge.

Alibainisha kuwa JKCI imeendelea kupanua huduma zake kwa kufungua matawi katika maeneo ya Kawe, Oysterbay, Kariakoo, Dar Group,  Arusha na Chato hatua inayolenga kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi. 

Dkt. Kisenge alisisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi, akieleza kuwa ni nguzo muhimu katika kuhakikisha huduma bora zinatolewa na maisha ya Watanzania yanaokolewa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa JKCI Dar Group  Dkt. Tulizo Shemu alisema mwitikio wa wananchi katika kupata huduma katika hospitali hiyo ni mkubwa hali inayoonesha hitaji la kuendelea kuboresha utoaji wa huduma.

“Kwa siku tunapokea wastani wa wagonjwa 500 wanaokuja kupata huduma katika hospitali yetu. Hivyo inawaomba wafanyakazi wote tujitume na kufanya kazi kwa ufanisi ili kukidhi mahitaji haya”, alisema Dkt. Shemu.

Naye Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  CPA. Agnes Kuhenga alisema pamoja na gharama kubwa za uendeshaji katika sekta ya afya, lengo la taasisi hiyo si kupata faida bali ni kuhakikisha inajiendesha kwa ufanisi na kumudu gharama za utoaji wa huduma.

“Ninawaomba wafanyakazi tushirikiane kutafuta njia za kupunguza gharama za uendeshaji ili taasisi iweze kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema CPA Agnes.

Nao  wafanyakazi wa taasisi hiyo wamepongeza utaratibu wa uongozi wa kuandaa vikao vya wafanyakazi vinavyowapa fursa ya kutoa maoni  huku wakisema hatua hiyo imeongeza uwazi, uwajibikaji  na ari ya utendaji kazi.

Tutazingatia maelekezo waliyopewa na viongozi wetu na kufanya kazi kwa bidii na kujituma, tutahakikisha tunatimiza majukumu yetu kikamilifu bila kuuangusha uongozi uliotuamini na kutupa nafasi ya kuwahudumia wananchi”, alisema Jilala John Afisa Ubora wa Huduma wa JKCI.

“Taasisi yetu  imejenga utamaduni mzuri wa kutushirikisha wafanyakazi katika taarifa za utekelezaji wa majukumu ya kazi, jambo linaloongeza uwazi na kuimarisha mazingira ya kazi. Tunajivunia kuwa sehemu ya taasisi hii, ushirikishwaji wa wafanyakazi ni mkubwa na unatupa motisha ya kufanya kazi kwa amani na ufanisi”, alisema Geraidina Karunde abaye ni mtunza kumbukumbu za wa Hospitali ya Dar Group.

“Ninawaomba wafanyakazi wenzangu kuzingatia maelekezo ya uongozi kwa kufanya kazi kwa bidii, kuwajibika na kulinda rasilimali za taasisi.Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunatekeleza maelekezo ya uongozi na kulinda mali za taasisi kwa manufaa ya wote”, alisema Abdul Mwinyi ambaye ni Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Hospitali ya Dar Group.