JKCI yawafanyia uchunguzi wa afya wafanyakazi 134 wa Bohari ya Dawa (MSD)
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Thursday, Jan 29, 2026
Wafanyakazi 134 wa Bohari ya Dawa (MSD) wamefanyiwa uchunguzi wa magonywa ya moyo, homa ya ini na Virusi vya ukimwi (VVU) na wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Uchunguzi huo umefanyika wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba iliyomalizika jana jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyakazi wa MSD wameishukuru Serikali kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuona umuhimu wa kufikisha huduma hizo mahali pa kazi na kutoa motisha kwa wafanyakazi kuchunguza afya zao.
Mfamasia wa MSD Peace Nyakojo alisema hatua ya kuwafuata wafanyakazi mahali pa kazi na kuwafanyia uchunguzi wa afya umewasaidia kwa kiasi kikubwa kufahamu hali zao za afya na kuchukua hatua za kujilinda dhidi ya magonja yasiyoambukiza.
“Naishukuru sana JKCI kwa kutufikishia huduma hizi, tumeelimishwa kuhusu hatari zinazoweza kuwapata wafanyakazi wa mijini na mambo mengine mengi, ninawaomba zoezi hili lisiishe hapa kwetu bali liweze kuwafikia wafanyakazi wenzetu waliopo katika kanda zote”, alisema Peace
“Nimefurahia huduma hii kwani tumezoea kupanga foleni hospitalini ili kupata huduma lakini leo bila foleni tumepata huduma kwa wakati, hata upande wa chanjo ya home ya ini hatukuwa tunaichukulia kwa umuhimu hadi baada ya kupata elimu ndio tumeona ni muhimu kupata chanjo hii”, alisema Norah Osei-Kumi, Mwanasheria wa Bohari ya Dawa (MSD)
“Tangu nimezaliwa sijawahi kupima afya ya moyo, changamoto za afya na vifo vya ghafla vimekuwa vingi hivyo inopotokea huduma kama hizi tusidharau tujitokeze kwa wingi kuchunguza afya zetu”, alisema Winifrida Milanzi, Afisa Ugavi wa Bohari ya Dawa (MSD).