Dkt. Pedro: Mwafrika wa kwanza kushinda tuzo ya kimataifa ya Moyo
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Friday, Dec 05, 2025
Mtanzania na Mwafrika wa kwanza kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Palangyo ameweka historia duniani baada ya kutunukiwa tuzo ya kimataifa ya Dr. Jay Brown International Best Abstract Award.
Mbali na tuzo hiyo Dkt. Pedro ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo wa JKCI pia ametunukiwa tuzo ya Paul Dudley White International Scholar Award ambayo haijawahi kutolewa kwa Mtanzania tangu ianzishwe.
Tuzo hizo zilitolewa katika Mkutano wa American Heart Association (AHA) uliofanyika hivi karibuni mjini New Orleans, Jimbo la Louisiana nchini Marekani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Dkt. Pedro alisema kutambuliwa kwake kimataifa kumetokana na utafiti wa miaka 10 uliofanywa na taassi hiyo kuhusu magonjwa ya moyo yanayoathiri uzazi, yanayojulikana kitaalamu kama Peripartum Cardiomyopathy (PPCM).
“Nimekuwa Mtanzania na Mwafrika wa kwanza na pekee kupata tuzo hizi mbili za heshima, baada ya utafiti wangu kutambulika kwa kiwango cha juu katika mkutano wa AHA. Hii ni kwa sababu ya ubora wa kisayansi, uvumbuzi, na athari za utafiti huu katika kuelewa magonjwa ya moyo yanayoathiri uzazi duniani,” alisema Dkt. Pedro.
Amefafanua kuwa ushindi wa tuzo hizo katika mwaka mmoja ni mafanikio makubwa na ya nadra, sio tu kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) bali pia kwa taifa, hatua iliyowashangaza wataalamu na wanasayansi wa kimataifa waliokuwepo kwenye mkutano huo.
Dkt. Pedro alisema kuwa ugonjwa wa PPCM ni nadra lakini hatari, na huwapata wanawake katika kipindi cha mwisho cha ujauzito au muda mfupi baada ya kujifungua.
“Utafiti huu wa muda mrefu umebaini kundi kubwa zaidi la wagonjwa wa PPCM duniani na umeleta mwanga mpya katika utambuzi, usimamizi na matokeo ya ugonjwa huu,” aliongeza.
Mafanikio hayo alisema yanaiweka Tanzania na Afrika Mashariki katika ramani ya kimataifa ya sayansi, hasa katika eneo la afya ya mama na magonjwa ya moyo.