• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Magonjwa ya kinywa yatajwa kuongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, Oct 09, 2025
image description

Magonjwa ya kinywa kwa watoto yakiwemo ya kuoza kwa meno na mafindofindo (Tonsillitis)  yanaweza kusababisha magonjwa ya valvu za moyo endapo hayatatibiwa kwa wakati.

Kauli hiyo imetolewa leo na Daktari wa Kinywa na Meno kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Aitham Mohamed, wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayoendelea katika Viwanja vya Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam.

Dkt. Aitham alisema kuna uhusiano mkubwa kati ya matatizo ya meno, kinywa na moyo, kwani kuharibika kwa meno husababisha kuwepo kwa bakteria ambao wanaweza kusambaa hadi kushambulia valvu za moyo na hivyo kusababisha magonjwa ya moyo.

“Tumekuwa tukiishauri jamii kulinda afya ya kinywa kwa kusafisha meno angalau mara mbili kwa siku. Hatua hii husaidia kuzuia kuharibika kwa meno na magonjwa ya kinywa yanayoweza kuhatarisha afya ya moyo”, alisema Dkt. Aitham.

Aliongeza kuwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua hupimwa afya ya kinywa kabla ya upasuaji, ili kuepusha maambukizi yanayoweza kusababishwa na bakteria baada ya upasuaji.

Kwa upande wake Daktari wa Upasuaji wa JKCI - Hospitali ya Dar Group Joyce Mkodo alisema katika kambi hiyo wataalamu wa upasuaji wameshiriki kutoa huduma kwa watu wenye changamoto za vidonda sugu.

“Tunafanya kambi hii kama sehemu ya kusherehekea mafanikio ya JKCI katika kipindi cha miaka 10 tangu ianze kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo. Wananchi wanapopata fursa kama hii wajitokeze kwa wingi, kwani wengi hawachunguzi afya zao hadi wanapopatwa na matatizo”, alisema Dkt. Joyce.

Dkt. Joyce aliongeza kuwa wagonjwa watakaobainika kuwa na matatizo ya kiafya watapatiwa rufaa kwenda Hospitali ya JKCI Dar Group iliyopo TAZARA kwa uchunguzi zaidi na matibabu.

Naye Ibrahim Ndube  mkazi wa Mbagala alisema amefurahia huduma hizo akibainisha kuwa ni faraja kubwa kuona taasisi kubwa kama JKCI inawafikia wananchi wa kipato cha chini.

“Huduma nilizopata hapa ni nzuri sana. Nimeonana na madaktari wa kinywa, mgongo na moyo. Nawapongeza kwa huduma bora na elimu nzuri kuhusu afya. Mtaji wa maisha ni afya, hivyo vijana wenzangu msisite kupima afya zenu”, alisema Ndube.

Kambi hiyo maalumu ya siku mbili inatoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo, sukari, shinikizo la damu, henia, vidonda vya muda mrefu, uti wa mgongo, maungio ya mifupa, pamoja na matibabu ya kinywa na meno.