• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

JKCI kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU) kuboresha matibabu ya moyo barani Afrika

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, Oct 09, 2025
image description

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inatarajia kusainimakubaliano maalumu na Umoja wa Afrika (AU) kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa wafanyakazi wa umoja huo ikiwemo kuwaleta baadhi ya wagonjwa wa moyo kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema taasisi hiyo itashiriki katika uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wafanyakazi wa Umoja wa Afrika (AU) pindi wanapofika hapa nchini kwa mikutano.

“Ujio wa ujumbe kutoka Umoja wa Afrika (AU) unaonesha namna Tanzania inavyotambulika kwa ubora wa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo barani Afrika. Tumetembelewa na kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali yetu chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan”, alisema Dkt. Kisenge.

Aliongeza kuwa baada ya kufanya tathmini ya kina, ujumbe wa Umoja wa Afrika (AU) uliridhishwa na ubora wa huduma, miundombinu, na wataalamu waliopo JKCI, na hivyo kukubali kuingia makubaliano maalumu ili taasisi hiyo iwe kituo cha kuwahudumia wafanyakazi wa Umoja wa Afrika na wananchi wa nchi mbalimbali barani Afrika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Huduma za Tiba kutoka Umoja wa Afrika (AU), Dkt. Adamu Isah, alisema wametembelea JKCI ili kutathmini uwezo wake na kujadiliana juu ya ushirikiano wa kimatibabu, na waliridhishwa na walichokiona.

“Tumevutiwa sana kiasi kwamba wafanyakazi wetu wa Umoja wa Afrika wataweza kupata huduma za matibabu ya moyo hapa bila kwenda Ulaya au sehemu nyingine,” alisema Dkt. Isah. 

Aliongeza kuwa hatua hii inapongeza uwekezaji mkubwa wa serikali ya Tanzania katika sekta ya afya na inapaswa kuigwa na nchi nyingine barani Afrika, huku ikilenga kutimiza dira ya Umoja wa Afrika ya “Afrika Tunayoitaka.”

Naye Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI Dkt. Tatizo Waane alisema ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na nchi jirani.

“Ziara hii ni sehemu ya kuunda mtandao wa huduma za afya barani Afrika, tukishirikiana na nchi jirani kama Zambia, Kongo, Zimbabwe, Kenya, Uganda na nyingine, katika kutoa huduma bora za magonjwa ya moyo,” alisema Dkt. Waane.

JKCI imeendelea kuwa kinara wa kutoa huduma za matibabu ya moyo barani Afrika, huku ikipokea wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali na ujio wa ujumbe wa Umoja wa Afrika (AU) unatarajiwa kuongeza ushirikiano na nafasi ya Tanzania kama kitovu cha ubora wa huduma za afya barani Afrika.