• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

JKCI yashinda tuzo ya uboreshaji wa huduma za matibabu ya moyo

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Tuesday, Aug 26, 2025
image description

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepata tuzo ya mshindi wa kwanza katika uboreshaji wa utoaji huduma za afya ikiwa ni ishara ya mafanikio yake katika kuboresha huduma za matibabu ya moyo nchini.

Tuzo hiyo imetolewa leo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango katika kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kinachofanyia katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kilichopo jijini Arusha.

Akizungumza wakati akikabidhi tuzo hiyo Mhe. Mpango aliipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa huduma inazozitoa za matibabu ya moyo kwa wagonjwa.

Akizungumza kabla ya kutolewa kwa tuzo hiyo ya uboreshaji wa utoaji wa huduma Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu alisema katika tuzo hizo walikuwa wanaangalia uboreshaji wa huduma na matumizi ya teknolojia ya kidijitali, kuridhika kwa wateja katika upatikanaji wa huduma na kuongezeka kwa wateja ambapo JKCI ilishika nafasi ya kwanza.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alishukuru kwa tuzo waliyopewa na kusema kuwa taasisi hiyo itaendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa inaowahudumia pia itaangalia namna itakavyozidi kutanua huduma zake.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema JKCI inashiriki katika kikao kazi cha tatu cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kwa kutoa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo.

“Viongozi wengi wana majukumu mengi ya kazi na kukosa muda wa kwenda hospitali kupima afya zao, wataalamu wa JKCI tumeona tuwafuate katika kikao hiki ili wakati wa mapumziko waje kupima afya za mioyo yao”.

Katika upimaji huu tunashirikiana na wenzetu wa Hospitali ya AICC na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kutoa huduma mbalimbali za matibabu na ushauri zikiwemo za moyo, ubongo, mgongo, viungo vya mwili, mifupa na mishipa ya fahamu pamoja na kufanya vipimo vya maabara ambapo majibu yao wanayapata ndani ya muda mfupi.

Dkt. Kisenge alisema wale wanaowakuta na shida wanawaanzishia matibabu kwa kuwapa dawa na wengine wanawapa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI au MOI kutokana na shida walizokuwa nazo.