Heart Team Africa Foundation Yalenga Kuokoa Maisha ya Watoto Wenye Magonjwa ya Moyo
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Wednesday, Jul 30, 2025
Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) imetoa wito kwa wananchi kuunga mkono taasisi hiyo kwakuchangia matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto na kuokoa maisha yao kwa wale wasioweza kumudu gharama za matibabu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) Mhe. Mussa Zungu huku wakiwa na jukumu la kusimamia na kuratibu mikatati ya kuwasaidia wanachi wenye matatizo ya moyo hususani watoto.
Akizungumza wakati wa mkutano wa taasisi hiyo hii leo Mwenyekiti wa Bodi ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) Mhe. Mussa Zungu alisema kuwa zaidi ya watoto 13,800 huzaliwa kila mwaka wakiwa na matatizo ya moyo na wengi wao hawana uwezo wa kugharamia matibabu hayo.
“Tunatakribani watoto elfu 13,800 kwa mwaka wanaozaliwa na shida ya moyo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anachangia asilimia 70 ya gharama za matibabu, gharama za kumtibu mtoto mmoja ni kati ya Shilingi milioni nane hadi tisa.” Alisema Mhe. Zungu.
Aidha, alieleza kuwa taasisi hiyo inawasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo kutokana na misaada ya wafadhili waliochangia zaidi ya Shilingi bilioni 3 na milioni 200 ili kusaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo.
“Bodi hii inaishi kutokana na michango ya wafadhili wa ndani na nje, tunawashukuru waliotuchangia bilioni 3 na milioni 200 kupitia harambee maalum ya kuchangia watoto wenye matatizo ya moyo,” aliongeza Zungu.
Mhe. Zungu alitoa wito kwa Watanzania kuungana na Serikali katika kusaidia juhudi za kuokoa maisha ya watoto kupitia mchango wao wa hiari.
“Hakuna sababu ya mtoto wa Kitanzania kufa kwa sababu ya ugonjwa wa moyo watanzania kushirikiana na Dkt. Samia na serikali yake tuunge mkono taasisi hii ili kuokoa maisha ya watoto wetu,” alisisitiza Mhe. Zungu.
Nae Mtendaji Mkuu wa Heart Team Africa Foundation Dkt. Naizihijwa Majani alieleza kuwa katika mkutano huo wamejadili mkakati wa miaka minne wenye lengo la kusaidia wagonjwa wa moyo na kuisaidia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na taasisi nyingine katika tafiti kuhusu magonjwa ya moyo.
“Leo tumepitia mpango mkakati wa miaka minne na wa mwaka mmoja jukumu letu kubwa ni kukusanya fedha kusaidia wasiokuwa na uwezo kwenye matibabu ya moyo na kufanya tafiti ili kusaidia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na taasisi nyingine,” alisema Dkt.Naiz.
“Tutaendelea kutoa elimu ya magonjwa ya moyo kwa jamii na pia kuwajengea uwezo watumishi wa afya kutoka hospitali ya JKCI ili kuwasaidia watoto na watu wazima wanaopata matibabu ya moyo,” aliongeza Dkt.Naiz.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge alieleza kuwa uanzishwaji wa HTAF ni sehemu ya mkakati wa kusaidia watoto wasiokuwa na uwezo wa kulipia gharama za matibabu ya moyo.
“Katika watoto 100 wanaozaliwa nchini kati ya mmoja au wawili huwa na magonjwa ya moyo na wengi hawana uwezo wa kulipia gharama za matibabu ndiyo maana bodi ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete iliridhia kuanzishwa kwa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) ili kusaidia watoto hao,” alisema Dkt. Kisenge.
“Moja ya malengo yetu makubwa ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu afya ya moyo, kuhamasisha watu kuchangia ili kusaidia wasiokuwa na uwezo wa kulipia gharama za matibabu ya moyo,” aliongeza Dkt.Kisenge.
HTAF imeahidi kuendelea kushirikiana na wananchi pamoja na wadau wote wa afya ili kuhakikisha watoto wote wenye matatizo ya moyo wanapata matibabu, bila kujali uwezo wao wa kifedha.