JKCI kutumia akiliunde kumtambua mtu kama atakuwa na magonjwa ya moyo baada ya miaka 10 ijayo
Author:JKCI Admin
Published At:Wednesday, Jul 30, 2025
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kushirikiana na Kampuni ya AtheroPoint ya nchini Marekani kutumia akiliunde katika kufanya uchunguzi ambao utatambua hatari ya mtu kupata magonjwa ya moyo na mishipa ya damu baada ya miaka 10 ijayo.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi hiyo Dkt. Angela Muhozya wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu ushirikiano unaokwenda kufanyika kati ya JKCI na kampuni hiyo.
Dkt. Angela alisema kupitia akiliunde wataweza kuzuia mtu kupata magonjwa ya moyo kwa kufanya vipimo vya moyo na mishipa ya damu na kutoa ushauri wa jinsi gani mtu anaweza kubadili mtindo wa maisha kwa kula vyakula bora, kufanya mazoezi, kutumia dawa stahiki kwa wale wenye magonjwa ya moyo tayari, kutokunywa pombe kupitiliza na kuacha kutumia bidhaa bidhaa hatarishi kwa mioyo yao kama tumbaku ambazo zinaathari kubwa kiafya.
‘’Teknologia hii ya akiliunde iliyojikita katika kuzuia magonjwa ya moyo ambayo itaanza kutumika katika taasisi yetu itatusaidia kuwafikia watanzania wengi zaidi kwa kufanya uchunguzi na kutambua magonjwa ya moyo miaka 10 kabla ya mtu kupata tatizo”, alisema Dkt Angela.
Dkt. Angela aliwaomba wananchi kufika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili waweze kukutana na teknologia hiyo iliyojikita zaidi katika kuzuia magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kwa kuwa wanaamini kinga ni bora zaidi kuliko tiba.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Radiolojia kutoka Wizara ya Afya Gelard Mrema alisema ushirikiano unaokwenda kufanyika baina ya JKCI na kampuni ya AtheroPoint inayotumia akiliunde kutambua magonjwa ya moyo na mishipa ya damu utawasaidia watanzania wengi kufahamu hali za mioyo yao zitakavyokuwa miaka 10 ijayo.
“Sisi kama Wizara tumeona tija ya kuleta kampuni ya AtheroPoint kwenye Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete kwani wanateknlolojia ambayo itaweza kumchunguza mgonjwa atakuwa na shida gani ya moyo na mishipa ya damu baada ya miaka 10 ijayo, huduma hii itapatikana JKCI siku chache zijazo”, alisema Mrema.
Naye Mkurugenzi kutoka kampuni ya AtheroPoint ya nchini Marekani Dkt. Jasjit Suri alishukuru kupata fursa ya kutoa elimu ya matumizi ya akiliunde katika kutambua magonjwa ya moyo katika miaka 10 ijayo na kuahidi kushirikiana na taasisi hiyo ili waweze kufikia maono yao ya kutoa huduma bora na za kisasa za matibabu ya moyo na mishipa ya damu.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inazidi kuimarisha utoaji wa huduma bora na za kisasa za matibabu ya moyo nchini lengo likiwa ni watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi wafikiwe na huduma za ubingwa bobezi za matibabu ya moyo.