• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Watu 1,369 wafanyiwa uchunguzi wa moyo maonesho ya Sabasaba

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Wednesday, Jul 30, 2025
image description

Watu 1,369 wakiwemo watu wazima 1,289 na watoto 80 wamepata huduma za  uchunguzi na matibabu ya moyo katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa maonesho ya Sabasaba yaliyomalizika hivi karibuni.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi hiyo Anna Nkinda wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma walizozitoa katika maonesho hayo.

Anna alisema baada ya kufanyiwa vipimo vya moyo na kupata matibabu, watu 217 walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kufanyiwa uchunguzi wa kina zaidi ambapo watu wazima walikuwa 209 na watoto 8.

“Watu 371 walifanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na watu 336 walifanyiwa kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo, vipimo vya maabara vilifanyika kwa watu 763 ambao walichunguzwa matatizo ya figo, ini, kiwango cha mafuta mwilini, pamoja na homa ya ini”.

“Watu 145 walipata elimu ya mtu mmoja mmoja ya ushauri wa lishe na kufuata mtindo bora wa maisha kutoka kwa mtaalamu wetu wa lishe ambao utawasaidia kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo”, alisema Anna.

Anna aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya za mioyo yao hasa pale ambapo taasisi hiyo inakuwa ikitoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo katika program yake ijulikanayo kwa jina la Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services.

Kwa upande wa wananchi waliopata huduma katika banda hilo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kujua afya za mioyo yao zikoje.

“Sijawahi kupimwa moyo katika maisha yangu, baada ya kusikia huduma ya upimaji inapatikana katika maonesho ya Sabasaba niliona nami nije kupima, nashukuru sana moyo wangu uko salama. Nimepewa ushauri wa jinsi ya kuutunza ili usipate madhara siku za mbeleni”, alishukuru Amon Mwasote mkazi wa Mkuranga.

“Mwanangu alikuwa na tatizo la kutokukua vizuri na kuchoka haraka anapocheza na wenzake, nilimpeleka katika hospitali kadhaa kutibiwa lakini hakupona, baada ya kufanyiwa vipimo amekutwa na tatizo la tundu kwenye moyo. Amepewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI”, alisema Jemima Masanja mkazi wa Morogoro.

Katika maonesho hayo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ilishika nafasi ya mshindi wa pili katika kundi la watoa huduma za afya.