Watoto 39 wafanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Saturday, May 17, 2025
Watoto 39 wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo ya siku tano iliyomalizika jana jijini Dar es Salaam.
Upasuaji huo umefanywa kwa watoto waliokuwa na magonjwa mbalimbali ya moyo ikiwemo mishipa mikubwa ya moyo kutoka sehemu isiyo sahihi, matatizo ya mishipa ya moyo ya upande wa kushoto na kulia, na matundu kwenye moyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Mkurugenzi wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema kambi hiyo maalumu ilikuwa ikifanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Mending Kids International la nchini Marekani.
“Watoto 22 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na watoto 17 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab, pia tumeweza kudumisha mahusiano na kuzidisha ujuzi katika kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela alisema kupitia ujuzi wanaoupata kutoka kwa wataalamu wengine ikiwemo Shirika la Mending Kids International wameweza kufanya upasuaji wa moyo na kuvuka mipaka ya Tanzania ambapo sasa wanatoa huduma katika nchi za Cameron, Morocco, Zambia na nchi nyingine lengo likiwa kujengeana uwezo na wataalamu wengine ili kwa pamoja waweze kuokoa maisha ya watoto wenye magonjwa ya moyo.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka nchini Marekani Sasha Agati alisema Mending Kids International imekuwa ikishirikiana na JKCI zaidi ya miaka 10, ambapo sasa mafanikio yamekuwa makubwa hivyo kuifanya taasisi hiyo kuwa bora barani Afrika.
Ushirikiano wetu mzuri umesaidia kuwaleta wagonjwa kutoka nchini Cameron kuja kufanyiwa upasuaji wa moyo hapa JKCI, ambao baada ya kufika wamefurahia kuona kuna nchi ipo Afrika na ina ujuzi mkubwa wa kufanya upasuaji wa moyo”, alisema Dkt. Sasha
Naye Daktari bingwa wa Upasuaji wa moyo kwa watoto kwa kutumia mtambo wa Cathlab wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Deogratius Nkya alisema kupitia kambi hiyo wataalamu wanaofanya upasuaji wa tundu dogo wameweza kuwafanyia upasuaji wa moyo bila kufungua kifua watoto 16 waliokuwa na matatizo ya moyo ya mishipa ya damu kuziba pamoja na matundu kwenye moyo.
Dkt. Nkya alisema watoto waliofanyiwa upasuaji katika kambi hiyo wapo ambao tayari wamesharuhusiwa na wengine wanaoendelea kupata matibabu wanendelea vizuri.
“Ni imani yetu kuwa wataalamu hawa wa Mending Kids International wataendelea kushirikiana nasi katika kutoa matibabu ya hali ya juu na kuboresha afya za watoto watanzania na wa Afrika.