Watu 383 wachunguzwa moyo Singida
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Monday, May 05, 2025
Watu 383 wamepata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu iliyofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) mkoani Sungida.
Huduma hiyo ya upimaji ilitolewa bila malipo katika maonesho ya Kimataifa ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali Pa kazi yaliyomalizika jana katika viwanja vya Mandewa mkoani Singida.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kambi hiyo daktari bingwa wa magonjwa yatokanayo na kazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Elius Birago alisema walitoa huduma za uchunguzi, matibabu na ushauri wa magonjwa ya moyo kwa watu wazima 364 na watoto 19.
“Watu 44 wakiwemo watu wazima 42 na watoto wawili tuliwakuta na matizo makubwa ya moyo yakiwemo ya kuziba kwa mishipa ya damu, umeme wa moyo na valvu, wagonjwa hawa wanahitaji kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu ya kibingwa tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi yetu”.
“Kwa upande wa jinsia wanawake walionyesha mwitikio mkubwa zaidi kwani walikuwa 258 na wanaume 125 hali hii ni kiashiria cha ongezeko la uelewa wa umuhimu wa kupima afya miongoni mwa wanawake ukilinganisha na wanaume”, alisema Dkt.Birago.
Dkt. Birago alisema katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo Taasisi hiyo inatoa huduma ya kuwafuata wananchi mahali walipo ijulikanayo kwa jina la Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan huduma hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwani watu wengi wamepata nafasi ya kupima afya za mioyo yao na kupata matibabu bila malipo yoyote yale.
“Ninaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwasomesha wataalamu wetu na kununua vifaa tiba vya kisasa na hivyo wananchi wengi zaidi kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo. Ninawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kupima afya zao pale watakaposikia kuna kambi za matibabu ya moyo kwa kufanya hivyo watatambua afya za mioyo yao na kuanza matibabu mapema kwa wale watakaokutwa na matatizo”, alisema Dkt. Birago.
Nao wananchi waliopata nafasi ya kupima afya zao walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kufahamu hali za mioyo yao na kujua jinsi gani wanaweza kujilinda ili wasipate magonjwa ya moyo.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kupima moyo, nashukuru kwa huduma niliyoipata nimepata huduma ya kiwango cha juu bila kulipa fedha yoyote ile, nimeelekezwa jinsi ya kufuata mtindo bora wa maisha unavyoweza kunisaidia nisipate magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo”, alishukuru Joseph Chacha mkazi wa Mandewa.
“Mwanangu akicheza na wenzake anachoka haraka na kutokwa na jasho jingi pia ukuaji wake ni wa shida, aliwahi kuandikiwa kufanya vipimo vya moyo lakini sikuwa na uwezo wa kulipia. Baada ya kusikia wataalamu wa moyo wako hapa nikaona nimlete baada ya kupima amekutwa na shida nimepewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI”.
“Ninawashukuru wataalamu wa moyo kwa kumtibu mwanangu na kugundua tatizo alilokuwa nalo ninaamini atatibiwa na atapona, ninawaomba kinamama wenzangu ambao hawana uwezo wa kifedha wasikate tamaa bali wawe na ujasiri pindi wakisikia kuna madaktari wako katika maeneo yao wanafanya kambi za matibabu waende kupata huduma kama nilivyofanya mimi”, alishukuru Asha Shabani mkazi wa Iramba.
Huduma zilizokuwa zinatolewa katika maonesho hayo ni za upimaji wa shinikizo la damu, kiwango cha sukari kwenye damu, kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, kipimo cha mfumo wa umeme wa moyo, uwiano baina ya urefu na uzito, elimu ya lishe bora, ushauri wa kiafya kuhusiana na magonjwa ya moyo ikiwemo matumizi sahihi ya dawa na ushauri wa magonjwa yatokanayo na kazi.