JKCI yatumia akili mnemba na teknolojia za kidijitali katika matibabu ya moyo
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Monday, May 05, 2025
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kuwa mstari wa mbele katika matumizi ya teknolojia za kisasa katika kuboresha huduma za afya kwa wagonjwa wa moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Hayo yamesemwa na daktari bingwa wa magonjwa yatokanayo na kazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Elias Birago wakati wa Maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) yaliyomalizika leo mkoani Singida.
“Matumizi ya akili mnemba na teknolojia za kidijitali katika kuimarisha usalama na afya mahali pa kazi, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete imekuwa kinara wa kkwa kuhakikisha tunatangulia mbele kutumia teknolojia hiyo kwa ufanisi mkubwa”, alisema Dkt. Birago.
Dkt. Birago aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia yamewezesha kupanua wigo wa utoaji huduma na kuweza kuwafikia wagonjwa walioko mbali na hospitali kwa kutumia tiba mtandao.
“Tumekuwa tukitumia teknolojia ya tiba mtandao kwa ajili ya kuwafikia wagonjwa wetu ambao wapo nyumbani huku sisi tukiwa ofisini, wagonjwa wanaotumia teknolojia ya tiba mtandao wanapata huduma zile zile kama ambavyo wangefika hospitali”, alisema Dkt. Birago
Dkt. Birago amebainisha kuwa mbali na tiba mtandao, JKCI inafanya uchunguzi wa mwenendo wa shinikizo la damu la mgonjwa kwa kutumia teknolojia ya kifaa cha DOZEE ambacho kinamwezesha daktari kufuatilia hali ya mgonjwa akiwa mbali.
“Teknolojia hii ya Dozee inatumika mgonjwa akiwa nyumbani na daktari akiwa hospitali anaweza kuona taarifa muhimu za mgonjwa kama mapigo ya moyo na shinikizo la damu (BP) kupitia mfumo huu wa kidijitali,” alisema Dkt. Birago.
Hatua hii ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono serikali ya awamu ya sita na kuhakikisha teknolojia inatumika kikamilifu katika utoaji wa huduma za afya hasusani katika magonjwa ya moyo.