Watoto 40 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa hayo ambapo 21 kati yao wamefanyiwa upasuaji wa moyo kwa kutumia tundu dogo (Minimum Invasive Surgery) katika kambi maalum ya matibabu ya moyo iliyofanywa na wataalamu wa  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la  Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo ya watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya kIkwete (JKCI) Stella Mongella ambaye pia ni mratibu wa kambi hiyo ya matibabu ya siku tano iliyoanza tarehe 28/3/2022 na kumalizika tarehe 1/4/2022.

Dkt. Stela alisema watoto waliofanyiwa uchunguzi na waliotibiwa ni wale wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni mishipa ya damu ya moyo  na matundu kwenye moyo. Hali za wagonjwa zinaendelea vizuri na kuna ambao tayari wamesharuhusiwa kurudi nyumbani na wengine wataruhusiwa wakati wowote kuanzia sasa.

Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya moyo ya watoto alisema uchunguzi huo pamoja na tiba ulifanyika kwa njia ya upasuaji wa bila kufungua kifua kwa kupasua sehemu ndogo kwenye paja kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambayo ni maabara inayotumia mionzi maalum kwa ajili ya uchunguzi wa matatizo na tiba za magonjwa ya moyo.

“Faida za upasuaji wa aina hii ni  mtoto anakaa wodini siku chache kwani baada saa moja baada ya  upasuaji anaweza kula chakula na baada ya  siku moja anaruhusiwa kurudi nyumbani, vifaa vinavyotumika kuziba matundu ni vya kisasa na ni salama kwa ukuaji wa mtoto. Pia watoto wanaofanyiwa upasuaji wa aina hii hawahitaji kufanyiwa  upasuaji mkubwa wa kufungua kifua”, alisema Dkt. Stela.

Dkt. Stela alisema watoto ambao walifanyiwa uchunguzi na hawakufanyiwa upasuaji ni wale ambao walikuwa na uzito mdogo pia kutokana na umri wao kuwa mdogo waliachwa ili matundu hayo yaweze kujiziba yenyewe kwani kuna matundu ambayo yanaweza kuziba kabla ya mtoto kufikia umri wa miaka mitano.

“Katika kambi hii tulimfanyia upasuaji mtoto aliyekuwa na umri wa miezi minne ambaye alikuja kama dharula kutokana na mshipa wake unaotoa damu kwenye moyo kupeleka  kwenye mapafu kuziba kabisa kwa asilimi 100 na hivyo kuhitaji matibabu ya dharula”,.

“Wakati tunamfanyia upasuaji tulikutana na changamoto ya mapigo ya moyo kwenda haraka sana na wakati mwingine kuwa chini tunamshukuru Mungu tulimfanyia upasuaji salama hivi sasa anaendelea vizuri na ananyonya vizuri”,alisema Dkt. Stela.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka hospitali ya Wolfson iliyopo nchini Israel Assa Sagi alisema katika kambi hiyo licha ya kufanya matibabu kwa watoto pia walitoa mafunzo kwa wataalamu wa JKCI ambao wanafanya upasuaji huo wa kuzibua mishipa ya damu na kuziba matundu ya moyo kwa watoto.

“Ninawashauri wazazi wakiona mtoto haongezeki uzito, anapumua kwa shida midomo yake na vidole  imebadilika rangi  na kuwa rangi ya bluu wasichelewe, wampeleke hospitali mapema ili akafanyiwe vipimo na kupata matibabu kwani wakichelewa mtoto anaweza kushindwa kutibiwa”, alisisitiza Dkt. Sagi.

Naye Simon Fisher ambaye ni Mkurugenzi Mtedaji wa Shirika hilo la SACH alisema tangu mwaka 1999 walianza kuja nchini kutoa huduma ya matibabu ya moyo kwa watoto lakini kutokana na janga la UVIKO - 19  lililoikumba Dunia mwaka 2020 hawakuweza kuja, lakini sasa hivi wamekuja  na kukuta badadiliko makubwa ya vifaa tiba vilivyopo JKCI hii ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa mtambo mpya wa kisasa wa Cathlab na  mtambo wa Carto 3 System 3D & Conventional  System.

“Nimefurahi kuona mashine ya Intra-Aortic balloon pump kwani kuwepo  kwa kifaa hiki kinachotumika kwa ajili ya wagonjwa ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo lakini mioyo yao ufanyaji wake wa kazi uko katika kiwango cha chini hivyo  basi anawekewa kifaa hiki ili kuusaidia moyo kufanya kazi kabla na wakati wa upasuaji kutawasaidia  wataalamu kufanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa na wagonjwa kupata huduma ya matibabu kwa wakati”, alisema Fisher.

Fisher alisema Shirika hilo litaendelea kutoa vifaa tiba pamoja na wataalamu ambao watakuja  nchini kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto pia kwa kushirikiana na wataalamu waliopo JKCI wanatarajia kwenda kutoa huduma ya matibabu ya moyo na mafunzo katika Hospitali ya moyo iliyopo nchini Zambia. 

Nao wazazi ambao watoto wao walitibiwa katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa baada ya watoto hao kufanyiwa upasuaji wameona mabadiliko kwa watoto hii  ikiwa ni pamoja na kuhema vizuri, kucheza vizuri na kula chakula vizuri tofauti na ilivyokuwa kabla hawajapata matibabu .

Loveness Ngowi alisema mwaka 2020  mtoto wake akiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi miwili  aligundulika kuwa na tatizo la ugonjwa wa moyo baada ya kuona mtoto anahema vibaya na anapata tatizo la ugojwa wa nimonia mara kwa mara alimpeleka hospitali na kufanyiwa vipimo ambavyo vilionesha ana tundu kwenye moyo.

“Baada ya kufanyiwa upasuaji  na kuzibwa tundu lililokuwepo kwenye moyo mtoto anacheza vizuri, anakula na anahema vizuri tofauti na ilivyokuwa kabla ya kupata huduma hii. Ninawashauri wanawake wenzangu wakiona mtoto hakui vizuri, anashindwa kuhema na anachoka haraka wakati anacheza wwampeleke hospitali mapema ili aweze kupata matibabu”, alisema Loveness.

Mama Tatu Mbaruku ambaye mjukuu wake alifanyiwa upasuaji wa kuziba tundu la moyo anasema mtoto alipokuwa na umri wa miaka miwili alikuwa na tatizo la kukohoa , maumivu kwenye mbavu na  kuchoka baada ya kufanyiwa vipimo aligundulika kuwa na shida ya matundu mawili kwenye moyo na kuandikiwa dawa za kutumia.

“Baada ya kuanza kutumia dawa hali ya mtoto ilibadilika na kuendelea vizuri. Alifanyiwa tena vipimo  ambavyo vilionesha tundu moja limeziba na kubakia tundu moja ambalo limezibwa jana baada ya kufanyiwa upasuaji mdogo wa moyo sasa hivi anaendelea vizuri”, alisema Mama Tatu.