Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeahidi kushirikiana na Hospitali za mikoa  ya  Mtwara, Manyara na Tanga kwa kuwatuma wataalamu wake kwenda kutoa huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo katika Hospitali hizo ili kusogeza huduma  karibu zaidi na wananchi.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati akiongea na viongozi wa Hospitali za mikoa ya Mtwara, Manyara na Tanga waliofanya ziara ya kikazi ya mafunzo ya siku tatu katika Taasisi hiyo.

Prof. Janabi alisema ziara ya viongozi hao imewasaidia  kujifunza na kujionea kwa macho huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

“Tutakuja kuwatembela katika Hospitali zenu, tutaona huduma mnazozitoa  na tutashirikiana kwa pamoja kutoa huduma kwa wananchi. Taasisi yetu imekuwa ikienda katika Hospitali mbalimbali za mikoa kutoa huduma za  matibabu ya moyo kwa wananchi kwa siku za mbeleni nanyi mtakuwa miongoni mwenu”, alisema Prof. Janabi.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake Mganga Mfawidhi  wa Hospitali ya mkoa wa Manyara Dk. Catherine Magali  aliishukuru Taasisi hiyo kwa kuwapokea na kuwapongeza  kwa huduma bora wanazozitoa kwa wagonjwa wanaowatibu.

Dk. Magari alisema katika ziara hiyo wamejifunza jinsi ya kuwajibika na kutoa huduma nzuri kwa mgonjwa hata kama mtoa huduma halipwi chochote.

“Kuwepo kwetu kwa siku tatu katika Taasisi hii tumejifunza na kujionea jinsi mgonjwa anavyopokelewa, kwenda kulipia bili, kwenda kwa daktari, kufanyiwa vipimo na kupewa dawa  kwa wakati hakuna kuchelewa katika kupata huduma. Nasi tutaenda kuyafanyia kazi haya tuliyoyaona katika Hospitali zetu”, .

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tiba Shirikishi wa Taasisi hiyo Dk. Delila Kimambo aliwashauri viongozi hao kuzingatia usafi katika Hospitali zao na kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wagonjwa kwani hakuna mtu ambaye anapenda kulipia huduma mbaya.

Dk. Delila alimalizia kwa kuwasihi viongozi hao kuvitunza vizuri vifaa vya Hospitali zikiwemo mashine vinavyotolewa na wafadhili ili viweze kutumika muda mrefu kwa kutoa huduma kwa wagonjwa.

 Katika ziara yao ya mafunzo ya siku tatu viongozi hao wa Hospitali za Manyara, Tanga na Mtwara walitembelea maeneo mbalimbali ya Taasisi hiyo na kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.

  • Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Hospitali za mikoa ya Mtwara, Manyara na Tanga mara baada ya kumalizika kwa ziara yao ya kikazi ya mafunzo ya siku tatu katika Taasisi hiyo.