Uingereza Yajiunga na Mataifa Mengine Kusaidia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa Kutoa Mafunzo Maalum Katika Upasuaji wa Moyo kwa Watoto

Madaktari Bingwa wa upasuaji wa Moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Chain of Hope la nchini Uingereza wamefanya upasuaji wa kufungua kifua kwa watoto tisa wenye umri wa miezi mitatu hadi miaka 17 kuanzia tarehe 23/07/2018 hadi leo tarehe 27/07/2018.

Watoto waliofanyiwa upasuaji ni wale wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambapo madaktari  wanatengeneza valve na kuziba matundu, kurekebisha mishipa ya moyo ambayo imekaa vibaya, kurekebisha mfumo wa uzungukaji wa damu katika moyo na kuweka valvu za bandia kwa wale walio na valvu za moyo zilizoharibika.

Wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji hali zao zinaendelea vizuri na sita  kati yao wameruhusiwa kutoka  katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kupelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu.

Kambi hiyo inaenda sambamba na utoaji wa elimu pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi kwa wataalamu wetu. Katika kambi hii Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto ni mwanamke hii imeleta hamasa kwa madaktari wetu wa kike kusomea upasuaji wa moyo ambapo kwa Tanzania hatuna Daktari wa kike wa upasuaji wa moyo wote ni wanaume.

Hii ni kambi ya tatu ya matibabu ya moyo kwa watoto tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2018 na ni mara ya kwanza kwa Uingereza kuja hapa nchini. Kambi nyingine zilizofanyika ni za upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua ambayo tuliifanya na wenzetu kutoka Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart-SACH) ya nchini Israel na Kituo  cha Moyo  cha Berlin (Berlin Heart Center) ya nchini Ujerumani katika kambi hii jumla ya watoto 17 walipata matibabu. Upasuaji wa kufungua kifua tulifanya  na wenzetu wa Taasisi ya Open Heart Internartional  (OHI)ya nchini Austarial na kufanya upasuaji kwa watoto 20. 

Kwa upande wa  wamama wajawazito ni muhimu wakafanya  uchunguzi (Fetal Echocardiography) wa kuangalia kama mtoto aliyeko tumboni anamatatizo ya moyo au la. Hii itasaidia kama mtoto anamatatizo ya moyo kupata matibabu mapema pindi atakapozaliwa.

Kama mnavyofahamu matibabu ya moyo ni ya gharama hivyo basi tunaendelea kuwahimiza wananchi  kujiunga na Mifuko ya Bima za Afya.