Jumla ya ndugu wa wagonjwa 95 wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanyiwa uchunguzi wa viashiria vya magonjwa ya moyo bila malipo pamoja na kupewa elimu ya jinsi ya kuyaepuka magonjwa hayo wakati wa  maadhimisho ya siku ya moyo Duniani. Kati ya ndugu hao wa wagonjwa waliofanyiwa vipimo asilimia 50 walikutwa na uzito mkubwa, asilimia 20 walikutwa na shinikizo la juu la damu ambapo asilimia tano walianzishiwa dawa za kutumia.  Akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam Dkt. Alexander Morosso alisema wagonjwa wengine sita wamekutwa na matatizo yanayohitaji uchunguzi zaidi na hivyo wameanzishiwa kliniki. “Asilimia kubwa ya watu tuliowapima walikutwa na tatizo la uzito mkubwa hii inaonesha kuwa watu hawafanyi mazoezi na kutozingatia lishe bore hivyo basi tumewashauri wapunguze kula vyakula vyenye mafuta, kuthibiti uzito wa mwili na kufanya mazoezi angalau dakika 30 kila siku”,

“Wote tuliowapima siku ya leo tumewashauri wawe na tabia ya kupima afya zako mara kwa mara ili kujua hali zao za  afya na kugundua mapema kama kuna tatizo kwani wengi tuliowapima na kuwakuta na matatizo hawakuwa wanajuwa kuwa wanamatatizo ya shinikizo la juu la damu”, alisema Dkt. Mrosso. 

Kwa upande wake Afisa Lishe wa Taasisi hiyo Husna Faraji alisema katika upimaji huo wametoa elimu ya jinsi ya  kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo kwa kufuata mtindo bora wa maisha ikiwa ni pamoja na kutmia maziwa yaliyopunguzwa au kuondolewa mafuta, kupunguza ulaji wa nyama nyekundu, hususan zenye mafuta, kula zaidi nyama ya kuku au samaki na kuepuka kula  vyakula vilivyokaangwa au vyenye mafuta kama soseji, nyama ya  kusaga,  keki, maandazi, vitumbua na viazi vya kukaanga.

“Nimewashauri kina mama wabadilishe njia ya kupika vyakula badala ya kukaanga wachemshe, wapike kwa mvuke, kuoka au  kuchoma na watumie  mafuta kidogo wakati wa kupika pia waongeze ulaji wa vyakula vya jamii ya kunde, mbogamboga na matunda. Pia waongeze  matumizi ya nafaka hasa zile zisizokobolewa kama unga wa dona, unga wa atta, ulezi na mtama”,alisema Husna. 

Aidha Husna aliwashauri  kupanga  shughuli ambazo watazifanya kila siku kwa kutembea kwa miguu, kutumia  njia ndefu ya kutembea badala ya ile ya mkato, kupunguza muda wa kutazama televisheni na kufanya shughuli zinazotumia viungo vya mwili kama kufua, kuosha vyombo, kuosha gari, kusafisha nyumba, kazi za bustani, kufyeka majani, kutumia redio, kwani mara nyingi unaweza kufanya shughuli mbalimbali huku ukisikiliza redio, kuepuka msongo wa mawazo, kuepuka uvutaji wa sigara au utumiaji wa tumbaku na kuepuka au kupunguza matumizi ya pombe. 

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano  wa Taasisi hiyo Anna Nkinda alisema kila mwaka maadhimisho ya siku ya moyo hufanyika tarehe 29 mwezi wa tisa ambayo kwa mwaka huu ni siku ya jumapili. Lakini kwa kuwa Taasisi hiyo kwa mwaka huu ilipanga kufanya upimaji kwa ndugu wa  wagonjwa wanaowatibu  na siku ya jumapili hakuna kliniki ya wagonjwa wa nje  ikaona ifanye upimaji huo siku ya jumamosi tarehe 28/09/2019. 

“Katika kuadhimisha siku ya moyo Duniani tumefanya upimaji wa urefu na uzito, tumeangalia uwiano baina ya urefu na uzito, tumepima kiwango cha sukari kwenye damu msukumo wa damu mwilini (BP) na kutoa dawa kwa watu waliokutwa na matatizo. Tumetoa elimu ya jinsi ya kuepuka magonjwa ya moyo na lishe bora kwa wagonjwa kwa kuwa ndugu wa wagonjwa ndiyo wauguzaji tukaona nao tuwafanyie upimaji na kutoa elimu kwao ambayo itawasaidia kufahamu magonjwa wa moyo”, alisema Anna. 

Nao ndugu wa wagonjwa ambao wamefanyiwa upimaji  pamoja na kupewa elimu waliishukuru Taasisi ya Moyo kwa huduma hiyo kwani wao kama wauguzaji wa wagonjwa ni muhimu wakafahamu ugonjwa ya moyo pamoja na lishe bora kwa wagonjwa. Alishukuru Zuhura Issa, “Mama yangu anatibiwa katika Taasisi hii, baada ya kusikia leo tunafanyiwa upimaji nimefurahi kwani nami nimepata faida ya upimaji pamoja na elimu. Ninaomba upimaji kama huu uwe unafanyika mara kwa mara”, 

Kila mwaka tarehe 29 mwezi wa tisa  huwa ni maadhimisho ya siku ya moyo Duniani ambapo wadau mbalimbali wanafanya upimaji  kwa wananchi pamoja na kutoa elimu kuhusu magonjwa hayo. Kauli mbiu ya mwaka huu ni : “Kwa moyo wangu, kwa moyo wako, sote pamoja kwa mioyo yetu , tunatimiza ahadi”.