Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imejipanga  kutanua huduma zake  kwa kutoa  matibabu ya moyo kwa kuwafuata wananchi wenye matatizo hayo katika hospitali za kanda zilizopo hapa nchini.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati akiongea na ujumbe kutoka jimbo la Shandong lililopo mjini Beijing nchini China waliotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa.

Prof. Janabi alisema Tanzania ni nchi kubwa na ina idadi kubwa ya watu hivyo basi ili huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo ziweze kuwafikia wananchi wengi zaidi  ni lazima wawafuate katika Hospitali za Kanda.

“Lengo letu la baadaye ni kuhakikisha huduma tunayoitoa katika Taasisi yetu inawafikia wananchi wengi zaidi wenye matatizo ya moyo walioko mikoani pia kutoa mafunzo kwa madaktari walioko katika hospitali za Kanda kwa kufanya hivyo tutasaidia wagonjwa wa moyo kupata matibabu kwa wakati”, alisema Prof. Janabi.

Aidha Prof. Janabi alisema tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo mwaka 2015 idadi ya wagonjwa wa moyo wanaokwenda kutibiwa  nje ya nchi imeweza kupungua kutoka wagonjwa 159 kwa mwaka 2012 hadi kufikia wagonjwa wawili kwa mwaka 2017.

Prof. Janabi alimalizia kwa kuzitaja changamoto zinazoikabili Taasisi hiyo kuwa ni pamoja na  kutokuwa na nafasi  ya kutosha kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hii ni kutokana na idadi ya wagonjwa kuongezeka kutoka wagonjwa 100 kwa mwaka 2016 hadi  kufikia wagonjwa 300 kwa mwaka 2018 .

Aliomba Taasisi ipatiwe nafasi za mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa wafanyakazi wake pamoja na kuongezewa idadi ya madaktari  bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka nchini China ambao Serikali ya nchi hiyo inawatuma kufanya kazi katika Hospitali mbalimbali hapa nchini ikiwemo JKCI.

Kwa upande wake Gavana wa Jimbo la Shandong Yu Xiao – ming aliipongeza Taasisi hiyo kwa huduma bora ya matibabu ya moyo wanayoitoa kwa wananchi na kuahidi kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha watanzania wanakuwa na afya njema ya moyo.

Yu Xiao - ming alisema magonjwa ya moyo ni moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza lakini yanawasumbua  watu wengi  ila kama yataweza kudhibitiwa mapema kwa watu kupewa elimu na kufanya upimaji wa afya zao mara kwa mara itasaidia wananchi kutoyapata magonjwa hayo kirahisi.

“Hivi karibuni jimbo letu limesaini mkataba wa kushirikiana na Taasisi hii, nitakahikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kwa wakati hii ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya  kuongeza idadi ya madaktari wa China kuja kufanya kazi hapa na kutoa mafunzo  ya muda mrefu na mfupi kwa wafanyakazi wa Taasii hii”, alisema Yu Xiao - ming.

Mwezi wa nane mwaka huu Taasisi hiyo ilisaini mkataba wa kushirikiana na jimbo la Shandong na Hospitali ya magonjwa ya Moyo ya Fuwai iliyopo mjini Beijing nchini China wa  kutolewa kwa  mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa wafanyakazi  na kufanya kambi maalum za matibabu ya moyo ambazo zitasaidia kuwajengea uwezo wataalam wa afya.