Ugonjwa wa Shinikizo la juu la damu hutokea wakati nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa ya moyo kuwa  kubwa kuliko kawaida. Ongezeko hilo husababisha moyo kufanya kazi kupita kiasi ili kusukuma  damu katika mishipa ya damu. Kwa kawaida ugonjwa wa shinikizo la damu halina dalili, ila likidumu kwa muda mrefu bila tiba lina madhara makubwa kiafya. Kuna aina mbili za  ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ambazo ni  shinikizo la juu la damu la kurithi na shinikizo la damu linalosababishwa na magonjwa mbalimbali. Asilimia 95 ya wagonjwa  wa shinikizo la juu la damu hawana sababu inayoweza kujulikana kisayansi. Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu halina sababu inayoeleweka na mara nyingi inaweza kusababishwa na mgonjwa kuwa na historia ya ugonjwa katika familia yao, uzito mkubwa kupindukia, matumizi ya chumvi nyingi, kutofanya mazoezi, uvutaji wa sigara, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi na umri mkubwa. Asilimia kubwa ya watu wanaopata  ugonjwa wa shinikizo la juu la damu huwa katika kundi hili na magonjwa mbalimbali kama  figo, mishipa ya moyo na  mfumo wa homoni. Aina hii ya shinikizo la juu la damu  huathiri asilimia 5 ya wagonjwa wenye  shinikizo. Kwa mfano aina hii ya Shinikizo la damu huweza kuwatokea kinamama  wakati wa ujauzito  na hupona  mara baada ya kujifungua.Kwa wagonjwa waliotibiwa  katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tangu ilipoanzishwa Septemba 2015 hadi Aprili 2020 kati ya wagonjwa 334,774 tuliowatibu asilimia 66 ya wagonjwa  walikuwa na tatizo la ugonjwa wa shinikizo la juu la damu. Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu unaweza kusababisha mwili kupooza,kiharusi (stroke), shambulio la moyo (Heart attack), moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure), kufanya moyo kuwa mkubwa, ugonjwa  wa figo na kupunguza nguvu za kiume. Unaweza kuepuka kupata ugonjwa wa shinikizo la juu la moyo kwa kufanya mazoezi,  kuzingatia  lishe bora kwa kula  matunda, mboga mboga, vyakula vyenye madini ya potassium vile vile kupunguza kula vyakula vyenye kiasi kikubwa cha mafuta  na chumvi. Kuepuka uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri, kutambua  kiwango cha sukari katika mwili wako, kutambua msukumo wako wa damu na kiwango cha mafuta mwilini.

“Tambua msukumo wako wa damu mwilini, (Blood Pressure – BP)”.