Wafanyakazi wa Taasisis ya Moyo Jakaya Kikwete wametakiwa kufanya kazi zao kwa umoja, kuwasaidia wahitaji na kuwatendea haki wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

Rai hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Idara Kuu ya Afya Dkt. Zainab Chaula alipokuwa akizungumza  na wafanyakazi wa Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.

Dkt. Chaula alisema kazi ya kuwahudumia wagonjwa ni ngumu na ni ibada hivyo basi kutokana na matendo mema watakayowatendea wagonjwa ambao ni wahitaji Mwenyezi Mungu atawalipa kwa  kuwajalia afya njema ili waweze kuwahudumia kwa miaka mingi zaidi.

“Nawapongeza sana kwa kazi mnayoifanya ya kuwahudumia wagonjwa  wenye matatizo ya moyo, kazi hii ni  ngumu jambo la muhimu ni kuwa na upendo  baina yenu na wagonjwa mnaowahudumia. Hakika Mwenyezi Mungu atawalipa kwa huduma yenu mnayoitoa”, alisisitiza Dkt. Chaula.

Alimalizia kwa kuwataka wafanyakazi hao kufanya kazi zao  kwa bidii, wakati  na kutimiza wajibu  wao kwani hakuna  kisichowezekana katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa vitu  vyote vipo ndani ya uwezo wao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi alimshukuru Katibu Mkuu huyo kwa kutembelea Taasisi hiyo na kuona huduma za matibabu ya moyo wanazozitoa.

Prof. Janabi  alisema idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo imekuwa ikiongezeka siku hadi siku na kutoa mfano wa wagonjwa wa nje 8557 waliotibiwa mwezi wa kwanza ukilinganisha na wagonjwa 7222 waliowaona mwezi wa Desemba mwaka jana.

Alisema   idadi ya wagonjwa wanaolazwa imeongezeka kutoka wagonjwa 282 kwa mwezi wa kumi na mbili mwaka jana hadi kufikia 312 waliolazwa mwezi wa kwanza mwaka huu.

“Tunaona wagonjwa kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na Visiwani ila wagonjwa wetu wengi zaidi wanatoka katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Mbeya, Arusha, Dodoma, Geita, Iringa, Kagera, Pemba,Katavi, Kigoma Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mara, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida,Tanga na Unguja ”, alisema Prof. Janabi.

  • Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimwelezea Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara kuu ya Afya, Dkt. Zainab Chaula jinsi duka la dawa linavyohudumia wagonjwa wa moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo wakati wa ziara yake ya kutembelea taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
  • Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara kuu ya Afya Dkt. Zainab Chaula akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa ziara yake ya kutembelea Taasisi hiyo leo kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo wanazozitoa.
  • Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara kuu ya Afya Dkt. Zainab Chaula akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa ziara yake ya kutembelea Taasisi hiyo leo kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo wanazozitoa.